HASHIL Seif Hashil alizaliwa kwenye ngarawa katika maji ya bahari ya
Pemba Januari 12, 1938. Alisoma skuli ya msingi ya Mkwajuni na baadaye
katika iliyokuwa Seyyid Khalifa Secondary Technical School, Beit-el-Ras,
Unguja. Alikuwa ni mmoja wa vijana wafuasi wa Abdulrahman Babu
waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi kabla ya Mapinduzi ya Januari
12, 1964. Baada ya Mapinduzi alipelekwa Indonesia kusomea sayansi ya
ubaharia kwa miaka miwili na pia alipelekwa China kusomea
uanamaji.Hashil Zanzibar alifanya kazi mbalimbali aliwahi kuwa afisa wa
tatu katika meli za MV Africa na MV Jamhuri. Alipouliwa Rais wa
Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume 1972, Hashil alikamatwa na kuwekwa
jela ya Ukonga, Dar es Salaam, kwa muda wa miaka sita. Alipofunguliwa
alikwenda Denmark kama mkimbizi. Baada ya miaka mitano akawa raia wa
Denmark. Alifanya kazi katika meli mbalimbali za Kideni na baadaye
alifanya kazi kwa miaka 20 katika Shirika la Haki za Binadamu la
Denmark. Hashil ni mshairi na mwandishi wa vitabu vya riwaya.